Friday, 20 September 2013

ANDREW KWAYU; Mwalimu wa Hawa Ghasia aliyezipaisha Ndanda, Azania, Ilboru




Na Mwandishi Wetu
KATI ya wakuu wa shule ambao ukipata nafasi ya kuzungumza nao utagundua kuwa wamestaafu kwa mafanikio na kwa heshima kubwa, Andrew Aseri Kwayu (pichani) ni mmoja wao.
Huyu ni Mkuu wa Shule mstaafu wa sekondari za Ndanda ya Masasi, Mtwara, Azania ya Dar es Salaaam ya Ilboru ya Arusha .
Mzee Kwayu anasema miaka 34 ya utumishi wa umma ilikuwa yenye mafanikio makubwa. Ingawa amestaafu, anasema hiyo ni kwa mujibu wa sheria tu, kwani bado anapenda kufundisha.
“Nilistaafu Septemba mwaka 2009. Lakini kwangu naona kama inanilazimu, kwa sababu ni utaratibu, kwani bado napenda kufundisha.  Naamini nitarejea kwenye ulingo kwa sababu zaidi ya kupenda kufundisha, bado nina nguvu na uwezo wa kufanya kazi hiyo ,” anasema kwa kujiamini. Kwayu ni mwalimu wa masomo ya Sayansi hasa Kemia.
Alianza kufundisha mwaka 1975 Sekondari ya Tosamaganga, Iringa. Akiwa hapo, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kemia mara baada ya kuripoti kazini na baadaye kuwa Makamu Mkuu wa Shule.
Anasema licha ya Tosamaganga kuwa mbali na mji na nyumbani kwao Kilimanjaro, ilimlazimu kwenda. “Unajua kipindi chetu tulikuwa na nidhamu sana, tofauti na vijana wa sasa, ambao ukiwapangia maeneo ya vijijini wanakataa kwenda.
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lilitusaidia sana. Na kwa sababu hiyo sikuona shida kwangu kwenda Tosamaganga,” anaeleza. Anasema kazi ya ualimu inahitaji moyo wa kujitolea na kujituma.
“Kweli maslahi ni madogo, lakini ukiipenda utaifanya kwa moyo na utafurahi kuifanya,” anasema.
Mwaka 1985 alipandishwa cheo na kuwa Mkuu wa Shule na kuhamishiwa Ndanda, Masasi. Anasema mtu yeyote anapopandishwa cheo hufurahi, lakini furaha yake ilizidiwa na changamoto alizozikuta Ndanda.
Anasema Ndanda kulikuwa na changamoto kubwa, moja ikiwa ni uhaba wa walimu. “Ingawa Serikali ilikuwa ikipanga walimu kwenda, lakini wengine walikuwa wakikataa au kuhama. Kwa hiyo changamoto kubwa kwangu ilikuwa ni kuwafanya walimu wakae.
“Ilinibidi nianzishe hafla za walimu. Hii ilinisaidia sana, kwani walimu walijiona ni kitu kimoja na kujenga hali ya kusaidiana panapotokea shida,” anasema.
Anaongeza kuwa “kuwafanya walimu wakae na kufurahi kwa pamoja ni kitu kizuri sana katika utawala. Lazima wakuu wa shule wawe wabunifu na kuwa karibu na walimu wakati wa shida na raha. Na nimekuwa nikijenga hali hiyo katika shule zote ambazo nikuwa naongoza.”
Kuhusu mafanikio aliyoyapata katika kipindi chote cha utumishi hasiti kutaja mafanikio waliyonayo wanafunzi wake. Anasema wamempa heshima kubwa katika jamii na humfanya awe mtu mwenye furaha sana.
“Kila sehemu ninayokwenda ndani ya Jiji hili, nakutana na wanafunzi wangu. Wengi wao nimekwishawasahau, lakini wao hunikumbuka na kunikumbusha.
Ninapokuwa ndani ya gari naendesha, hunipigia honi na ninapoegesha mjini na kutembea kwa miguu, hunilazima kusimama mara kwa mara kusalimiana nao. Kwa kweli huwa nafarijika sana na hali hii huniongezea siku za kuishi ,” anasema huku akitabasamu.
Kwayu amefundisha wanafunzi wengi lakini kati ya wachache anaowakumbuka ni Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mbunge wa Mtwara Vijijini akiwa Ndanda Sekondari. Wamo pia Dk. Marina Njelekela, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Muhimbili, Faustine Shilogile ambaye ni Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro na wengine wengi.
“Namkumbuka sana Hawa, alikuwa kiongozi mzuri sana tangu shule. Ni mmoja wa wanafunzi waliokuwa na uwezo mkubwa sana darasani. Huwa ananifanya nitembee kifua mbele,” anasema.
Anasema idadi kubwa ya wanafunzi anaowakumbuka ni wa Azania. Baadhi ya anaowakumbuka kwa majina ni Mathias ‘Kifimbo’ kwa sasa yuko Arusha, Innocent yuko Marekani, Mwita Mwikwabe aliwahi kuwa Rais wa Daruso (kwa sasa anafahamika kama Mwita Mwikwabe Waitara yuko Chadema), Humphrey Polepole na wengine ambao anawakumbuka kwa sura.
Anasema katika shule ambazo aliwahi kupitia, anasema Azania ndiyo shule ambayo aliifurahia sana kutokana na aina ya wanafunzi aliokuwa nao.
Anasema wanafunzi wa Azania walikuwa ni wa pekee sana na waelewa pia. “Niliwajengea umoja ambao ni ngumu kuuelezea. Nilikuwa nikijivuna kuwa na aina ile ya watoto na ndiyo hawa hawa ambao huwa nakutana nao katika ofisi mbalimbali.
“Nakumbuka hawa watoto alikuwa akiguswa mmoja inakuwa kama wameguswa wote. Walikuwa wakipendana na kushirikiana katika masomo na mambo mengine ya kijamii. Ilikuwa ni vigumu sana kumkuta mmoja yuko peke yake,” anakumbuka.
Anasema kilichokuwa kikimfurahisha zaidi ni uwezo mkubwa wa kitaaluma waliokuwa nao wanafunzi wa Azania. “Walinifanya nitembee kifua mbele kutokana na hilo.
Nami sikuwakatisha tamaa, nilihakikisha nawapa msaada wa kila aina wa kitaaluma na nidhamu. “Niliwapanga walimu wangu na kuwasimamia kuhakikisha kila mwanafunzi anapata kilichomleta shuleni, na hii ndiyo siri ya mafanikio ya shule yangu,” anasema.
Kila kazi ina changamoto zake. Ni vigumu kuwa kazini kwa kipindi cha miaka zaidi ya 30 ukose changamoto. Kwayu anasema amewahi kukumbana na matatizo mengi ambayo anayachukulia kama changamoto.
Kwanza anasema ilikuwa ugomvi mkubwa mwaka 1993 kati ya wanafunzi wa Azania na Tambaza.
Anasema chanzo cha fujo ilikuwa ni ushangiliaji wakati wa michezo ya UMISETA. Anafafanua kuwa katika kushangilia, wanafunzi wa Tambaza walimpiga mwanafunzi wa Azania. Siku iliyofuata, wanafunzi wa Azania walilipiza kisasi kwa kumpiga mwanafunzi wa Tambaza mitaani.
“Hapo ndipo ugomvi mkubwa ulipozuka, kwani Tambaza walitutafuta kulipiza kisasi. Wakati huu walikuja kutuvamia shuleni kwa lengo la kudhuru wanafunzi wetu na kuchoma maabara yetu ya Kemia,” anaeleza na kukiri kuwa hatasahau tukio hilo.
“Nakumbuka ilikuwa asubuhi ya saa nne. Wanafunzi wangu walikuwa darasani. Tulisikia mayowe na kelele kutoka kwa wanafunzi wangu kuwa tumevamiwa. Nilitoka nje, walimu na wanafunzi.
“Wanafunzi wa Tambaza walikuwa pembeni ya uwanja wetu wa mpira wa miguu wakiwa na chupa zilizokuwa na petroli. Walikuwa wanataka kuchoma maabara yetu ya Kemia. Mimi bila kutambua niliingia ndani ya maabara hiyo, lakini wanafunzi wangu walifanikiwa kunitoa,” anasema.
Anaongeza kuwa “baadaye tulifanikiwa kuwazingira na kuwadhibiti kwa kushirikiana na Polisi. Ulikuwa wakati mgumu sana kwangu. Lakini nashukuru yalikwisha.”
Tukio la pili analolichukulia pia kama changamoto kwake ni mgomo wa walimu mwaka 1995. “Mgomo huu ulikuwa ni changamoto kwangu, kwanza ulikuwa haramu kwa sababu hukufuata taratibu. Na kipindi hicho kulikuwa hakuna chama cha walimu.
Pili ulikuwa ukiratibiwa na mmoja wa walimu wangu, Peter Mashanga. Tatu ulipangwa kuanza siku ya kuanza mtihani wa kidato cha nne,” anaelezea.
“Nakumbuka nilifika ofisini saa 12 asubuhi na nilikuta Mashanga amefika tayari kuanza mgomo.
Nilichokifanya ni kuwa muwazi kwa walimu na kuwaeleza kuwa kazi yangu si kuwakataza kugoma, bali kumripoti yeyote ambaye hatafanya majukumu niliyompangia kama Mkuu wa Shule.
“Muda wa mtihani ulipofika, niliwapangia walimu wangu majukumu na wote wakaingia madarasani kusimamia mitihani, na hivyo kufanikiwa kuzima mgomo shuleni kwangu.”
Kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya wanafunzi wa shule za sekondari kugomea masomo na chakula. Mara nyingi migomo hii imekuwa ikiambatana na vurugu na uharibifu wa mali za shule.
Kwa kipindi chote cha miaka 24 ambacho amekuwa Mkuu wa Shule, Kwayu anasema haukuwahi kutokea mgomo wowote shuleni kwake.
Anasema migomo mingi inayotokea husababishwa na mawasiliano mabaya kati ya uongozi wa shule na wa serikali za wanafunzi.
“Ni muhimu sana kuwashirikisha wanafunzi kupitia serikali zao kile kinachoendelea katika shule. Kunapokuwa na mabadiliko yoyote, ni vizuri kuwajulisha,” anasema Kwayu. Anasisitiza kuwa “wakuu wa shule hawana budi kuwasikiliza wanafunzi.
Mimi utaratibu huu ulinisaidia sana na ndiyo maana haikuwahi kutokea migomo katika shule yoyote chini ya uongozi wangu. Niliwajengea wanafunzi wangu uwezo wa kujieleza na kuhoji jambo lolote wasilolifahamu.”
Anaongeza kuwa akiwa Azania, alianzisha gazeti la wanafunzi (Azania News Magazine) ambalo lilikuwa likitumiwa na wanafunzi kama uwanja wa kutoa mawazo yao.
“Walikuwa wanaandika mada mbalimbali wanabandika kwenye ubao maalumu kuhusu mambo yanayohusu shule na mengine yaliyokuwa yakitokea nje ya shule; ya kisiasa, kiuchumi au kijamii.
“Hii ilitusaidia sisi viongozi na walimu kwa jumla kujua nini kinaendelea shuleni, wanafunzi wanafikiria nini au wapi kuna upungufu. Walikuwa na Bodi ya Uhariri na walikuwa huru kuandika walichoona kina manufaa,” anasema.
Kumekuwa na taarifa katika vyombo vya habari kuwa baadhi ya walimu wamekuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi na wakati mwingine kusababisha wanafunzi kupata ujauzito.
Mwalimu Kwayu anasema tabia za namna hii zimekuwa zikidhalilisha taaluma ya ualimu. “Ni aibu sana kwa mwalimu kukumbwa na kashfa za namna hii.
Nafikiri ni wakati muafaka kufanya tathmini ya mitaala katika vyuo vyetu vya ualimu ili kufahamu chanzo.
“Lakini kwa kuanzia, ni lazima mwalimu ajitambue yeye kama mwalimu, nafasi na wajibu wake katika jamii, na pia mwanafunzi ajitambue pia na azingatie kilichompeleka shuleni. Katika kulifanikisha hili, walimu na wazazi hawana budi kushirikiana,” anasema.
Mwaka 2005 Mwalimu Kwayu alihamishwa kwenda kuwa Mkuu wa Sekondari ya Ilboru. Hii ni shule ya wanafunzi wenye vipaji vya pekee. Anasema changamoto kubwa aliyokabiliwa nayo ni kurudisha uelewano kati ya walimu na wanafunzi.
“Kabla yangu, kulikuwa na hali ya kutoelewana kati ya walimu na wanafunzi. Na ilishawahi kutokea wanafunzi wakaandamana kwenda kwa Mkuu wa Mkoa.
Hatua ya wanafunzi haikuwafurahisha walimu na hivyo kukawa na hali mgongano,” anaelezea. Kutokana na hali hiyo, hakukuwa na mabaraza ya wanafunzi.
Akiwa Mkuu Mpya wa Shule anasema wajibu wake mkubwa ulikuwa ni kuziweka sawa pande zote mbili.
“Ilinilazimu kuwa na mikutano ya mara kwa mara kati ya wanafunzi kwa wanafunzi, wanafunzi na walimu, serikali ya wanafunzi na walimu na walimu na walimu. Hii ilisaidia sana, kwani tofauti baadaye zilikwisha na sasa Ilboru hali imetulia,” anasema.
Licha ya kutokea kupenda ualimu, lakini anasema halikuwa chaguo lake la kwanza. “Kulikukwa na uhaba wa walimu na wahandisi katika miaka ya sabini mwanzoni. Ili kuondoa tatizo hilo kipaumbele kikubwa kilikuwa ni kupata walimu wengi na wahandisi.
Kwa hiyo ilinibidi nibadilishe mawazo na kusoma ualimu,” anasema. Mwalimu Kwayu alizaliwa Septemba 20, 1949 Machama-Nshara wilayani Hai, Kilimanjaro.
Alihitimu elimu ya msingi katika Shule ya Kati ya Nshara mwaka 1965. Baadaye alijiunga na Sekondari ya Malangari mkoani Iringa kuanzia mwaka 1966 hadi 1969.
Aliendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Mkwawa kuanzia mwaka 1970 hadi 1971, kabla ya kujiunga Chuo Kikuu kusomea Shahada ya Ualimu kuanzia mwaka 1972 hadi 1975 alipojiunga na JKT kambi ya Ruvu.
Ends

2 comments:

  1. Ninaafikiana na Kila Maelezo aliyoyatoa Mwalimu Kwayu. Jina langu Ni Thobias L. Marandu Nilikuwa Makamu Mwenyekiti shule ya Azania wakati nikiwa Kidato cha Pili. Innocent Mwesiga alikuwa ni Katibu wa shule na baadaye akawa Mwenyekiti wa shule. Hivi sasa Nipo Nchini Marekani, Nimekuwa hapa kwa miaka 14 kama Mkandarasi wa Umeme wa Viwandani sasa.
    Mwalimu Kwayu alikuwa ni Mkuu wa shule mwenye Uwezo Mkubwa sana wa Uongozi, Kuna Kipindi fulani tulikuwa tukifyeka majani kwa makwanja, Mw. Kwayu akaja pale akaomba kwanja akaanza kufyeka majani pamoja nasi huku akibadilishiana mawazo na sisi. Hii ilifanya Kila mtu kuanzia waalimu mpaka wanafunzi wamwone kama Baba na Rafiki. Alikuwa ni mtu asiyependa mzaha na Kazi lakini asiye na majivuno wala kujiona. Alikuwa na Utu sana, Siku Moja mimi na mke wangu tulitokea katika sherehe Gongolamboto, Mwal kwayu naye alikuwapo na mke wake. Tulipokuwa tukiondoka sisi tulitangulia na hatukuwa na gari yeye bila kunikumbuka akaja nyuma yetu, akasimamisha gari akatuchukua baada ya kufahamiana alionyesha furaha sana. Kwayu Ni Mtu muugwana sana simpambi ni kweli.
    Mimi naami kabisa Mwalimu Kwayu anao uwezo wa kuongoza watu na ni mbunifu sana. Anaweza Kuwa Kiongozi wa Ngazi yoyote ya Taifa na akaongoza kwa mafanikio makubwa.

    ReplyDelete
  2. Machozi yanaweza yakanitiririka kwa kusoma habari hii. Kwa jina naitwa Jumanne Mtambalike Trainee Manger Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia kwa kweli nilijifunza mambo mengi kwa mzee huyu. Siku zote alikuwa very loyal kwa wanafunzi wake.

    ReplyDelete