ELIMU ni nyezo muhimu katika
maisha ya binadamu. Kutokana na nguvu ya elimu katika kukuza uchumi wa nchi,
mataifa mengi duniani yaliyopata maendeleo ya kijamii na kiuchumi yamewekeza
katika sekta ya elimu.
Hakuna taifa lolote duniani ambalo linaweza kupata maendeleo bila watu wake kuwa na elimu na kwa maana hiyo hakuna maendeleo bila elimu. Elimu ndiyo inamfanya binadamu kuwa daktari, rubani, mhandisi na mtaalamu katika nyanja mbalimbali.
Kwa kutambua hilo, uwekezaji katika sekta hiyo umekuwa ukiongezeka. Leo hii kumesikika vilio vingi nchini vikilenga mazingira bora na fursa zaidi katika sekta ya elimu vinavyotokana na watu wengi kutambua nguvu ya elimu kwa vizazi vijavyo.
Mfuko wa Pensheni wa PPF kwa kutambua umuhimu wa elimu mwaka 2003 ulianzisha fao la elimu. Sababu ya msingi iliyousukuma Mfuko huo kuanzisha fao hilo ni kutokana na umuhimu wa watoto wa mwanachama kuendelea kupata elimu hata baada ya mzazi wao kufariki.
PPF ilianzisha fao hilo kwa kuanza na watoto watatu ambao wazazi wao walifariki wakiwa katika ajira na wamechangia mfuko huo kwa miaka mitatu au zaidi.
Kwa mwaka 2012 pekee Mfuko wa Pensheni wa PPF ulisomesha watoto 1,333 kwa kuwalipia jumla ya shilingi milioni 682 katika shule 765 kutoka Tanzania Bara na Visiwani katika shule za msingi na sekondari.
Fao hilo limewavutia wengi wanaotambua nguvu ya elimu na kujiunga na PPF ili waweze kufaidika na fursa zinazotolewa na Mfuko huo likiwamo fao la elimu linalotolewa baada mwanachama kufariki.
Kutokana na mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa fao hilo Mfuko wa Pensheni ya PPF uliadhimisha miaka 10 ya fao la elimu kama sehemu ya kutathmini mafanikio hayo katika Jiji la Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Salma Kikwete na kuhudhuriwa na baadhi ya watoto wanaofaidika.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio (pichani), anasema fao hilo ni kati ya mafao saba yanayotolewa na PPF. Anasema fao hilo hujumuisha ulipaji wa karo za shule na mahitaji mengine ya mwanafunzi husika kama vile sare, vifaa (stationaries), usafiri na chakula kwa kuzingatia mshahara wa mzazi aliyekuwa mwanachama wa PPF.
Erio anasema fao la elimu hutolewa kwa watoto wasiozidi wanne wa mwanachama aliyefariki akiwa katika ajira baada ya kuchangia katika mfuko huo kwa miaka mitatu au zaidi.
Mkurugenzi huyo Mkuu wa PPF anasema fao hilo lilianza kwa kusomesha wanafunzi watatu, lakini sasa idadi yao imekuwa ikiongezeka kila mwaka, ambapo Mfuko hulipia gharama ya ada kwa watoto wa mwanachama aliyefariki kuanzia elimu ngazi ya awali (chekechea) hadi kidato cha nne.
Anaeleza kuwa gharama za ada na matumizi mengine hulipwa moja kwa moja kwenye shule ambazo watoto wanasoma bila kupitia kwa mzazi aliyebaki au mlezi, jambo ambalo linatoa uhakika kwamba fedha zinatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Anatoa wito kwa wananchi kujiunga na PPF ili waweze kufaidika na mafao yanayotolewa na mfuko huo, likiwamo fao la elimu kwani limekuwa mkombozi kwa wanafunzi wengi nchini.
Anasema PPF imekuwa ikibeba majukumu ya mzazi ambaye amefariki akiwa kazini, kwa kuhakikisha watoto wake wanaendelea kupata elimu.
Akielezea historia ya Mfuko wa PPF, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, Erio, anasema Mfuko wa Pensheni wa PPF ulianzishwa mwaka 1978 kwa madhumuni ya kuandikisha wanachama, kukusanya michango, kuiwekeza pamoja na kulipa mafao.
Anasema PPF imekuwa inatekeleza majukumu hayo kwa ufanisi mkubwa kiasi kwamba idadi ya wanachama imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, pamoja na michango ya wanachama ikikua kila mwaka na mapato yanayotokana na uwekezaji nayo yakiongezeka.
Anafafanua kuwa mafanikio hayo
yamewezesha Mfuko kuwa na thamani ya shilingi trilioni 1.09 hadi kufikia
Desemba 2012.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa PPF, Profesa Adolf Mkenda, anasema waliamua kuanzisha fao hilo baada ya kugundua kuwa watoto wengi wa wanachama wao wanashindwa kuendelea na masomo baada ya wazazi wao kufariki kwa kushindwa kulipa ada za shule na mahitaji mengine muhimu.
"Hii ilichangiwa pia na ukweli kwamba wengi wa ndugu wa marehemu na wasimamizi wa mirathi walikuwa na vipaumbele vyao tofauti, ikiwamo kugawa urithi bila kujali umuhimu wa elimu kwa watoto waliobaki kwa kuwa jambo hilo halikuwa mojawapo ya vipaumbele vyao," alisema.
Anasema PPF kwa kutambua kuwa urithi mkubwa zaidi ambao mzazi anaweza kumwachia mtoto ni elimu, waliamua kuvaa viatu vya wazazi na kuwasomesha watoto hao ili kuwajengea mazingira bora.
Anaongeza kuwa mafanikio ya fao hilo hayapo tu katika idadi ya wanafunzi wanaowasomesha, bali pia katika matokeo ya mitihani yao baadhi ya watoto wanaofaidika na fao hilo hufaulu vizuri.
"Kwa mfano katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2011 na 2012 miongoni mwa wanafunzi waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza na la pili wapo wanaosomeshwa na PPF," anasema.
Anabainisha kuwa mbali na mafanikio hayo, pia fao hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo baadhi ya shule kushindwa kutuma ripoti za mitihani kwa PPF ambazo zingesaidia kutambua maendeleo ya wanafunzi hao, ili kujua namna bora zaidi ya kuboresha utoaji wa fao hilo.
Changamoto nyingine ni katika kupata uhakika kuwa wanaosomeshwa ni watoto wanaostahili na si watoto wengine kwa majina ya watoto wa marehemu, hivyo inalazimu PPF kufanya uhakiki wa mara kwa mara jambo ambalo ni gharama kubwa.
Prof. Mkenda anatoa changamoto nyingine kuwa ni waajiri kuchelewa kutuma taarifa za vifo vya wafanyakazi wao mara wanapofariki. "Hii inasababisha watoto wa marehemu wanachama kuchelewa kulipiwa ada, hususan pale kifo kinapotokea wakati mwaka mpya wa masomo unapoanza, jambo ambalo linaathiri uendelevu wa elimu ya wanafunzi.
"Hata hivyo Mfuko huo wa PPF utaendelea kukabiliana na chanagamoto hizo na kuhakikisha kuwa fao la elimu linatolewa kwa wakati na linaendelea kuwa bora zaidi," alisisitiza Prof Mkenda.
PPF inashauri Watanzania ambao hawajajiunga na Mfuko huu kufanya hivyo mapema ili waweze kuwa sehemu ya wale wanaofaidika na mafao yanayotolewa ikiwa ni pamoja na fao la elimu. Pia PPF itaendelea kuboresha huduma zake kwa wateja kama ilivyo kawaida yake katika kipindi cha miaka yote 35, tangu ilipoanzishwa.
*Raia Mwema, toleo Na. 294 la Mei
15, 2013
No comments:
Post a Comment